Taasisi ya Benki ya NBC Tawi la Songea imeamua kutoa sehemu ya mapato yake kwa kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi katika kituo cha kulelea watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi Matogoro Manispaa ya Songea.Pichani ni Sista Aloisia Mbunda (OSB) mlezi wa watoto akiwa na wafanyakazi wa NBC Tawi la Songea.
Benki ya NBC Tawi la Songea imeamua kutembelea jamii inayoishi katika mazingira hatarishi ili kuwatia moyo watoto wajione kama na wao ni sehemu ya Jamii ya Benki hiyo na wanastahili kuhudumiwa kupitia faida inayopatikana kutokana na watu kupata huduma katika Taasisi hiyo. Pichani Wafanyakazi wa NBC wakiwa katika kituo cha Nia njema cha watoto Yatima Matogoro.
Watoto wanaoishi katika kituo cha kulea Watoto wanaoishi katika mazingira Hatarishi Matogoro wamesema kituo chao kinakabiliwa na changamoto ya chakula, Sare za shule na Michango ya Hosteli na mahitaji mengine ya shule kama daftari na peni. Wameomba Jamii kuwakumbuka katika misaada mbalimbali ili kuwafanya watimize malengo yao ya kuendelea na elimu.
Benki ya NBC Tawi la Songea Imetoa Mahitaji yenye thamani ya Shilingi laki nne katiks kituo hicho cha Matogoro. Akikabidhi vifaa hivyo, Meneja wa Benki ya NBC Tawi la Songea Simon Ntwale amewataka watoto kuzingatia Elimu ili siku za baadae waondokane na utegemezi na kuwa mfano kwa jamii.
Benki ya NBC imekuwa ikisaidia vituo mbalimbali vya watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi, hivyo jamii nyingine inapaswa kuiga mfano huo badala ya kutumia pesa nyingi kwa ajili ya starehe na anasa wakati kuna watoto wanalala njaa.
Meneja wa Benki ya NBC Simon Ntwale amesema msaada walioutoa ni mdogo kwa mahitaji ya watoto katika kituo hicho ambapo pana watoto zaidi ya ishirini wanaosoma sekodari katika shule mbalimbali ni jukumu la kila mwanajamii kuunga mkono hatua hii.
Watoto wakipokea msaada wameushukuru uongozi wa Benki ya NBC kwa kuwakumbuka wamesema wamejiona na wao kama wako na wazazi pindi wanapotembelewa, wameahidi kuongeza bidii katika masomo wanachoomba ni msaada wa watu wenye mapenzi mema ili waweze kutimiza malengo yao.
watoto wanaoishi katika kituo cha Matogoro pamoja na kupata elimu na kutegemea misaada ya wahisani pia wanajiendeshea miradi ya ufugaji wa samaki, kilimo cha mahindi na kilimo cha miti ili kusaidia kupata baadhi ya mahitaji kupitia miradi hiyo.
Helena Kapinga na wenzake wakipokea chakula kutoka kwa wafanyakazi wa Benki ya NBC walipotembelea katika Kituo cha Kulea watoto yatima Matogoro Manispaa ya Songea
Sista Aloisia Mbunda (OSB) amesema kituo hicho zamani kilikuwa kinategemea wafadhili kutoka Ujerumani Uswis na Newsland ambao walikuwa wakitoa kiasi cha Dola 2000 mpaka 2500 ambazo zilikuwa zikisaidia kuwalipia ada na mahitaji watoto wa shule lakini kwa sasa baadhi ya wafadhili wamepungua baada ya kupoteza maisha hivyo waliobaki wanapata kama dola 800 hadi 1000 ambazo hazikidhi kwa mahitaji ya kituo.
Kituo cha Nia Njema Matogoro kinachomilikiwa na Sista Aloisia Mbunda (OSB) chini ya Kanisa Katoliki kinachukua watoto wanaomaliza elimu ya Msingi na wanaosoma shule za msingi kuwagharamia mahitaji ya chakula na shule kwa sasa kina watoto ishirini na mbili ambao wako sekondari lakini mpaka sasa baadhi ya watoto hawajaenda kuripoti shuleni kutokana na kusubiri ada ambapo kwa watoto wote kwa mwaka kituo kinahitaji si chini ya milioni 15 kulipia michango ya hosteli na mahitaji mengine ya shule.
Watoto waliolelewa katika kituo cha Kulea watoto waishio katika Mazingira Hatarishi Matogoro wapo waliofanikiwa kusomeshwa na sasa wana ajira katika Sekta mbalimbali zikiwemo Jeshi la Wananchi, Manesi , waalimu na wengine Seminari ambapo kwa sasa ni wahudumu katika madaraja ya ushemasi na uchungaji.
Wafanyakazi wa Benki ya NBC Tawi la Songea wakiwa katika kituo cha Matogoro wameguswa na hali ya kuwasaidika watoto kutokana na mafanikio yanayopatikana kupitia vituo vya kulelea watoto yatima, wamesema walezi wa vituo peke yao hususani masista hawawezi bila jamii kushirikiana na wamiliki wa vituo katika kuwasaidia watoto hao ambao hawana hatia na hawakupenda kuishi katika mazingira hayo.
Kutoa ni moyo na si Utajiri, hujafa hujaumbika, Ukitoa kwa watu wenye mahitaji maalum kama watoto waishio katika mazingira magumu Mungu atabariki, imezoeleka miaka hii watu huchangia zaidi katika mambo ya starehe kuliko kwa wenye matatizo. Pichani Meneja wa Benki ya NBC Tawi la Songea, Simon Ntwale akiwa ameshika mfuko wa unga wa kilo 50 ikiwa ni sehemu ya mahitaji waliyoandaa kwa ajili ya kuwakabidhi watoto wanaoishi kituo cha watoto yatima Matogoro Songea.
NBC iliweza kutoa Magodoro ya kulalia watoto wakati kituo cha Nia Njema Matogoro kinaanzishwa na mpaka sasa wamekuwa wakikitembelea mara kwa mara, pia wametembelea na vituo vinegine vikiwemo kituo cha Yatima cha Chipole Songea Vijijini na Kituo cha Mkuzo Manispaa ya Songea.
Sista Aloisia Mbunda (OSB) alipotembelewa na Meneja wa Benki ya NBC Tawi la Songea kwa lengo la kuwafariji watoto wanaoishi katika Mazingira Hatarishi.
Sista Aloisia Mbunda (OSB) Msimamizi wa watoto wanaoishi katika Mazingira Hatarishi Matogoro Songea akiwa na wafanyakazi wa Benki ya NBC Tawi la Songea walipotembelea kituoni hapo.
No comments:
Post a Comment