Wazee hao kutoka vijiji vya Makemba na Luhimba Kata ya
Mtyangimbole, Mzee Abdala Ally na Bibi
Paulina Nyoni wameiomba Serikali
iharakishe kutoa Pensheni kwa wazee wote ili kunusuru Maisha ya Wazee kwa
kukosa mahitaji ya chakula na dawa.
Babu Pius Mayumba pichani ndiye anayemtunza Bibi Paulina Nyoni mwenye umri wa 78 ambaye pia ni mgonjwa wa kifua kwa muda mrefu hawawezi kumudu gharama za Matibabu na usafiri kutoka nyumbani hadi hospitali umbali wa km 64.
Bibi Paulina Nyoni (78) Akiongea na Waandishi wa Habari walipomtembelea nyumbani kwake kutaka kujua changamoto anazokabiliana nazo na namna anavyoweza kumudu gharama za matibabu na hali anapoishi pamezungukwa na msitu yuko mbali na makazi ya watu wengine, amesema Analishukuru shirika la PADI kwa kumuibua na kuweza kuziainisha changamoto zinazomkabili zikiwemo na kushindwa kumudu gharama za matibabu na usafiri kwa kuwa kila anapokwenda Hospitali anatakiwa kulipa Sh. 5000 ili aweze kupata dawa. Pia mwendo wa kutoka nyumbani hadi Hospitali unamgharimu shilingi 2500 kwenda na kurudi ni sh. 2500.
Bibi Paulina Nyoni amesema yeye mwenyewe hawezi kwa kuwa hana msaada wowote na ugonjwa anaoumwa unahitaji kupata dawa kila mwezi licha ya changamoto zingine za chakula, mavazi na mahali salama pakuishi. Anadai ili apate matibabu inamlazimu awe na sh 10,000 kila mwezi za kuweza kukidhi kupata dawa na usafiri. Ameiomba Serikali kuharakisha uwezeshwaji wa kutoa Pesheni kwa wazee wote pengine akipata pensheni itamsaidia kupata matibabu.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Makemba Hassan Issa Kawenga alipoulizwa jitihada gani zinazofanywa na serikali yake katika kumuwezesha mahitaji Bibi Paulina Nyoni amesema Baada ya Shirika la PADI kukaa na Uongozi wa Serikali ya Mtaa na Wananchi kuhamasisha jinsi ya kuwasaidia wazee Mwaka huu wameazimia mara baada ya mavuno ya Msimu huu kila Mwananchi wa Mtaa wa Makemba kumchangia Bibi huyo kiasi cha kilo nne za mahindi ili ziwasaidie kwa ajili ya chakula.
Hiyo ni choo ambayo huitumia Bibi Paulina Nyoni na Mume wake ambaye naye ni mzee unaweza kustaajabu bibi ambaye hana uwezo wa kutembea na ni mgonjwa yuko katika hali ya kutetemeka muda wote anawezaje kuifikia choo hiyo na imekaa umbali mrefu kutoka kwenye nyumba ambayo anaishi na yenyewe si salama.
Bibi Paulina Nyoni akiwa anatoka ndani ya Nyumba anamoishi amesema kutokana na kukosa uwezo na msaada ameshindwa kutumia dawa kwa muda wa miezi minne sasa baada ya kukosa hela ya kuweza kumsaidia kupata Dawa na usafiri wa kufika Hospitali kwani hana uwezo wa kutembea umbali wowote zaidi ya kuingia ndani na kutoka nje.
Hayo ni Malazi ya Bibi Paulina Nyoni ambaye hana wasaidizi wa kumsaidia zaidi Jamii ilimtenga lakini kupitia Shirika la PADI inaendelea kuhamasisha jamii ya eneo hilo ili imsadie huduma ndogo ndogo kwa sasa walau watu wanajitokeza kumchotea maji na shughuli zingine ndogo ndogo. Jitihada zingine zinazofanywa na shirika la Padi katika kuwasadia wazee hawa ni kuhamasisha wadau kuchangisha fedha kwa ajili ya kuwajengea Nyumba ya kuishi ambayo itakuwa ni salama kwao.
Waandishi wa Habari wa Mkoa wa ruvuma na Viongozi wa Serikali ya Mtaa wa Makemba Kata ya Mletele walipomtembelea Bibi huyo kujionea changamoto anazozipata na jitihada zinazofanywa na shirika la kuhudumia Wazee la PADI katika kuwasaidia wazee hao akiwemo Bibi Paulina Nyoni.
Hilo Ndilo eneo ambalo anaishi Bibi Paulina Nyoni ambalo kwa mbali utaona limezungukwa na msitu hakuna Nyumba jirani. Swali la kujiuliza je endapo kunatokea shida za usiku na makazi ya ni ya aina hiyo wanawezaje kujinasua. Ni jukumu la Kila mdau kuguswa na Maisha ya Wazee hawa ambao wana mahitaji mengi Shirika la PADI peke yake halikidhi kuwafikia wazee wote wenye mahitaji ya aina hii. Pia Jamii inapaswa kutambua thamani ya wazee.
Shirika la PADI linalohudumia wazee Tanzania linafanya kazi kubwa ya kuwahudumia wazee na kuwaibua wenye mazingira hatarishi ili jamii iweze kuwasaidia na kuepukana na dhana mbaya kwa wazee kwa kukwepa Majukumu ya kuwahudumia. Piachani ni Afisa wa PADI Jackson akiingia ndani kumuona Mzee Abdalah Ally (77) ambaye anaishi kwenye nyumba hiyo na ni mgonjwa ambaye haamki kitandani kwa muda wa miaka 20 sasa katika Mtaa wa Luhimba Kata ya Mtwangimbole Madaba.
Mzee Abadalah ally akiwa amelala kitandani kwenye kibanda ambacho hakina hata dirisha na mlango. Amesema katika maisha yake hakuwahi kupata mtoto wala kuoa lakini alianza kuugua kwa muda mrefu zaidi ya miaka 20 sasa.
Mzee Abdala Ally anasema changamoto zinazomkabili ni kushindwa kutoka nje kwa kuwa hana uwezo wa kuamka haja zote anazipata akiwa kitandani ama kwa kuwekewa dishi na mtoto wa mdogo wake anayemtunza ambaye naye ana tatizo la Kifafa. Amesema endapo Serikali itatoa Penshen kwa wazee itamsaidia kukidhi baadhi ya changamoto.
Mganga Mkuu wa Zahanati ya Luhimba George Palangyo amesema changamoto kubwa inayojitokeza katika kumuhudumia mzee Abdalah Ally kwa watoa huduma wa wagonjwa wa Majumbani, ni kukosa vifaa vya kuweza kumsaidia katika kumuhudumia vikiwemo vifaa vya haja kubwa na ndogo na will chair ambayo ingeweza kumsaidi kumtoa nje na kupata hewa ya nje na mazoezi ya viungo.
Wazee wanahitaja msaada wa kila hali na mali toka kwa serikali, wadau na jamii kwa ujumla. hiyo ni hali ya choo ambacho kinatumika na mzee ambaye awali alikuwa na uwezo wa kufanya shughuli mbalimbali za ujenzi wa Taifa.
Pamoja na Changamoto zinazowakabili wazee wengi lakini wamesema wanaishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuonyesha nia ya kuwajali wazee wanachokiomba ni serikali kutunga sheria ya wazee ili iweze kuwalinda na kuwa salama katika maisha yao ya uzeeni.
Hiyo ni nyumba wanayoishi wategemezi wa Mzee Abdala Ally ambao na wao hawana uwezo na wana matatizo ya ugonjwa wa kifafa Unaweza kuona hii familia kwa ujumla ina hadha kwa kiasi gani. Shirika la PADI liliweza kumuibua Mzee huyu na kushirikisha HBC watoa huduma ya Afya Majumbani na kuanza kumtembelea kumfanyia usafi na kumnunulia Godoro la kulalia.
Mzee Abdalah Ally akiwa amelala ndani alipotembelewa na waandishi wa Habari na Uongozi wa Shirika la kuhudumia Wazee la PADI nyumbani kwake Lihumbu Kata ya Mtyangimbole.
Baadhi ya watoa huduma ya Afya na Majirani wa Mzee Ally Abadala. Kwa yeyeote mwenye kuguswa na maisha hayo anaweza kutoa mchango wa aina yheyote wa wazee hao kwa kupitia Shirika la PADI chini ya Mkurugenzi wake Iskaka Msigwa. Shirika la Padi limeanza taratibu za kuzijengea Nyumba familia hizo mbili kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali.